Zengwe kukwamisha Lowasa laja


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 27 May 2013

Printer-friendly version
Edward Lowassa

MKAKATI wa Edward Lowassa kutaka kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huenda ukakwama baada ya baadhi ya vigogo ndani ya chama hicho kupanga mkakati wa kutaka kumfukuza, imefahamika.

Taarifa za ndani ya CCM zinasema mpango wa kutaka kumfukuza Lowassa kutoka chama chake unatokana na hofu ya baadhi ya wagombea wenzake wanaohaha kutaka kumrithi Rais Jakaya Kikwete mwaka 2015.

Vyanzo vya habari vya MAWIO vimemnukuu mmoja wa vigogo waandamizi ndani ya chama hicho akisema, mkakati wa kumvua Lowassa uanachama unasukwa kwa ustadi mkubwa na kigogo mmoja mwandamizi mwenye ushawishi mkubwa ndani ya chama na serikali.

“Huyu bwana tayari ameanza mikutano ya kampeni, hata  kabla ya chama chetu kutoa mwongozo. Anazunguka nchi mzima kusaka urais. Huku ni kuvunja taratibu. Tutakutana na kumdhibiti,” ameeleza mtoa taarifa wa gazeti hili kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Taarifa zinasema mkakati wa kumfukuza Lowassa utaegemea hoja kuu mbili:

Kwanza, ni madai kuwa Lowassa ameanza kampeni kabla ya chama chake kutoa mwogozo; kujenga mtandao wa ushindi na kudaiwa kupanga safu za uongozi; jambo ambalo linaweza kukidhoofisha chama chake.

Kuhusu tuhuma za kuanza kampeni mapema, mtoa taarifa anasema, Lowassa anatuhumiwa, pamoja na mambo mengine, kuzunguka nchi nzima kufanya mikutano na baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), wenyeviti wa mikoa na makada wengine wa ngazi za kati na kuwashawishi kumuunga mkono katika mbio zake za kusaka urais.

Taarifa zinasema Lowassa alikutana na wajumbe wa NEC na baadhi ya wenyeviti wa mikoa ya Kanda ya Ziwa Vicktoria, tarehe 5 na 6 Mei 2013, mkoani Shinyanga.

Mwanasiasa huyo alikuwa mkoani Shinyanga alikokuwa miongoni mwa waalikwa kwenye sherehe za kuwekwa Wakfu Askofu Emmanuel Makala wa Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria - Shinyanga.

Hata hivyo, mkakati wa kumfukuza Lowassa kwa madai ya kuanza kampeni mapema waweza kukwama kwa kuwa mmoja wa wagombea anayepigiwa chapuo na walioko madarakani, naye tayari ameanza kampeni.

Pili, mkakati wa kumfukuza Lowassa, unatajwa kujikita kwenye madai ya kuhusika kwenye ufisadi wa mkataba tata wa kufua umeme wa kampuni ya Richmond Development Company (RDC).

Wakati mkabata huo unafungwa, Lowassa alikuwa waziri mkuu wa Jamhuri. Alitajwa na Kamati Teule ya Bunge, kwamba ndiye aliyeshinikiza watendaji serikalini kuipa kampuni hiyo kazi ya kufua umeme. Ilithibitika baadaye kuwa kampuni haikuwa na uwezo, ujuzi wala sifa ya kufanya kazi iliyopewa.

Mtoa taarifa anasema, ni mara baada ya mkutano wa Shinyanga ambapo taarifa zake zilivuja kwenye chama na serikalini na mpango wa kumfukuza ukafufuliwa upya.

Gazeti hili lilipowasiliana na kiongozi mmoja mstaafu serikalini kuhusu kufukuzwa kwa Lowassa na iwapo mkakati huo unaweza kufanikiwa, haraka alisema, “Hata mimi nimesikia. Nami nimewauliza kama ambavyo unaniuliza wewe, kwamba ‘mtaweza?’”

Anasema amewaambia kuwa huyu bwana (Lowassa) tayari amejijenga ndani ya chama na kwamba hatua yoyote ya kumfukuza sasa inaweza kukivuruga zaidi chama hicho.

Akiongea kwa hasira kigogo huyo alisema, “Huyu bwana (Edward Lowassa), anataka kutuharibia chama chetu. Lazima tumfukuze. Tutaitisha vikao vya Kamati Kuu (CC) na NEC kumjadili. Tunataka tulifanye hili kabla ya mambo kuharibika zaidi.”

Hata hivyo, wapinzani wa mkakati wa kumfukuza Lowassa wanasema, kufanikiwa kwa mpango huo kutakigharimu mno CCM kuliko kumuacha Lowassa hadi mwisho akapigiwa kura na kukataliwa na wajumbe wa vikao vya chama.

Katika mkutano wa Shinyanga, mtoa taarifa anasema, Lowassa alitangazia wafuasi wake kuwa ameanza mbio za kutafuta urais; aliahidi kupambana hadi mwisho.

“Nakuambia, kule Shinyanga Lowassa alitikisa. Ng’ombe sita wakachinjwa. Wajumbe karibu wote wa NEC kutoka Kanda ya Ziwa, walihudhuria. Wakuu wa wilaya wakafurika. Fulana zilizoandikwa Friends of Lowassa (Marafiki wa Lowassa), zikagawiwa. Nakuambia hakuna anayeweza kutuzuia tena mara hii,” ameeleza kada mmoja wa CCM ambaye ni shabiki wa Lowassa.

Kuibuka kwa taarifa hizi za kutaka kumdhibiti Lowassa kwa tuhuma za kuanza kampeni kabla ya muda, kumekuja wiki tatu baada ya gazeti hili kuanika orodha ya watu 14 wanaotajwa kutaka kuwania urais, miongoni mwao wakiwa wale wanaodaiwa kuwa tayari wameanza kampeni.

Miongoni mwa wanaotajwa kuanza kampeni, ni Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Mambo ya Ndani, Emanuel Nchimbi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Steven Wassira na aliyepata kuwa waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.

Katika mbio hizo, Membe anatajwa kuunganisha nguvu na Migiro kwa upande mmoja na Samwel Sitta kwa upande mwingine.

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, muungano kati ya Membe na Sitta unasukumwa na agenda ya kukabiliana na nguvu ya Lowassa.

“Hata muungano kati ya Membe na Migiro, nao ni kama muungano kati ya Membe na Sitta. Yote hii, inasukumwa na kukabiliana na Lowassa. Sasa ikitokea Lowassa akakatwa mapema, nao hawa wataanza kukimbiana, kila mmoja akitafuta urais kivyake. Maana wataona yule anayewanyima usingizi tayari atakuwa ameshaondoka,” ameeleza mtoa taarifa wetu.

Anasema, “Hata hawa, kama alivyo Lowassa, tayari wameanza kampeni. Mwishoni mwa mwezi uliopita, Membe alikuwa Iringa, ambako pamoja na mambo mengine alikutana na makundi mbalimbali ya watu na kutangaza kugombea urais,” ameeleza kigogo mmoja wa chama hicho kwa sharti la kutotajwa gazetini.

“Hata huyo Migiro, naye ameanza kampeni. Ngeleja ameanza kampeni. Mwakyembe ameanza kampeni. Wasira anazunguuka mikoani kujinadi na kusema kwamba ndani ya CCM kuna wagombea wawili tu – yeye na Lowassa. Lakini anasema, Lowassa jina lake halitapitishwa na Kamati Kuu, hivyo mgombea atakayebaki ni yeye,” anaeleza.

Kuhusu madai ya tuhuma za ufisadi, MAWIO limejulishwa kuwa tayari Lowassa amenasa taarifa kuwa kama mpango wa kumfukuza utakwama, basi nguvu itaelekezwa katika vikao vya mchujo kwa hoja kwamba ametuhumiwa kwa ufisadi na hivyo hauziki.

“Hizo habari, tayari zimemfika Lowassa mwenyewe. Nakuapia tutalipua bomu. Tunasubiri tuhuma hizo zililetwe ndani ya vikao vya chama wakati wa mchujo. tutaanika kila kitu. Lowassa ataeleza kila anachokifahamu kuhusu Richmond,” anaeleza mfuasi wa Lowassa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka CCM, akiwa mkoani Iringa, Membe alifanya mkutano na viongozi wa madhehebu ya kidini, wazee wa kimila na makundi mengine mbalimbali, kwa lengo la kujitambulisha.

Aidha, Membe alihudhuria kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa. Katika kikao hicho, Membe alinukuliwa akijigamba kuwa ni yeye anayeweza kutosha kupambana na yule wa upinzani, Dk. Willibrod Slaa, mgombea wa kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Mtoa taarifa wa gazeti hili amemnukuu Membe akisema, “Nimeongea na Rais Kikwete. Amesema bado dhamira yake iko palepale ya kukabidhi kijiti hiki cha urais kwa mwana-CCM mwenzake. Lakini ni mwanachama huyo asiyekuwa na chembe ya tuhuma za ufisadi,” ameeleza mtoa taarifa huyo akinukuu waziri Membe.

Akizidi kumnukuu Membe, mtoa taarifa anasema, “alituambia pamoja na rais kutamani kuacha uongozi wa nchi kwa mgombea wa chama chake, lakini sharti mtu huyo anayeachiwa asiwe na chembe ya harufu ya ufisadi.”

Mbali na Membe kufanya mikutano ya kampeni, amemwaga maelfu ya fulana zilizobandikwa picha yake upande wa mkono wa kushoto; tayari baadhi ya fulana hizo zimetawanywa kwa makatibu wa mikoa na wilaya.

Naye Dk. Migiro, taarifa zinasema alikutana na viongozi mbalimbali wa kidini kutoka madhehebu ya Kiislamu jijini Dar es Salaam kupanga mkakati wa urais.

Katika mkutano huo, vyanzo vya taarifa vinasema Dk. Migiro amenukuliwa akiwaambia kuwa ametumwa na mwenyekiti wa chama hicho kuwaambia kutangaza dhamira yake ya kugombea urais.

“Nimewaita kuwaambia kuwa nimetumwa na mwenyekiti, niwaambie kuwa ninayo nia... naomba mniunge mkono,” amenukuliwa akisema kiongozi mmoja wa kidini ambaye alidai kuwa miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo.

Anasema, “Sisi tukamuuliza, utaweza? Mbona Edward (Edward Lowassa), ameshamaliza kila kitu? Naye akajibu, “Nami naona hivyo. Lakini nimehakikishiwa na mwenyekiti,” ameeleza mjumbe huyo akinukuu Dk. Migiro.

Lowassa, ndiye alikuwa makamu mwenyekiti wa kile kilichoitwa, “Mtandao wa Kikwete 2015,” jambo ambalo wachambuzi wa mambo wanasema limempa uzoefu mkubwa wa kujenga mitandao ya ushindi nje ya mfumo wa chama.

Kundi la wanamtandao ndilo linalodaiwa kufanya kazi kubwa – chafu na safi – katika kufanikisha mbio za urais wa Kikwete mwaka 2005.

Lowassa ndiye alitajwa kuwa mratibu mkuu wa kundi hilo. Wajumbe wengine walikuwa Rostam Aziz, Membe na Sitta.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: