Zigo la posho ni la ikulu


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 08 February 2012

Printer-friendly version
Uchambuzi

KADRI mjadala wa nyongeza ya posho za vikao kwa wabunge unavyozidi kupamba moto, ndivyo wananchi nao wanavyozidi kuona tatizo linavyokua, na si ufumbuzi.

Katika mjadala huo kupitia vyombo vya habari na vikao vya wabunge, umma umelishwa mengi, ikiwemo kwamba Rais Jakaya Kikwete hajaidhinisha posho hizo bali alichokifanya ni kulipeleka suala hilo kwa wabunge waliamue.

Kwa upande mwingine, umma umeaminishwa kuwa posho hizo zilianza kulipwa mkutano uliopita. Wengine wamesema hazijalipwa, isipokuwa fedha walizowekewa wabunge kwenye akaunti zao ni za malipo ya vikao vya mwisho wa wiki walivyoshiriki kwa mkutano uliopita.

Posho zinazoibua mjadala ni za vikao zilizotajwa kuongezeka kutoka Sh. 70,000 hadi Sh. 200,000 kwa siku.

Kwa ongezeko hilo, ina maana wabunge wanapokuwa vikaoni sasa wapokee hadi Sh. 330,000 kwa siku. Zaidi ya zile Sh. 200,000; kuna malipo ya Sh. 80,000 na nauli Sh. 50,000 ziitwazo “posho ya kujikimu.”

Wakati viongozi wa bunge, Spika Anne Makinda na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah wakipingana kimsimamo; Ikulu inazidi kumtua mzigo Rais kuwa hajabariki posho mpya.

Hata hivyo, taarifa hiyo ya Ikulu inakiri Rais anakubali haja ya posho kwa wabunge kuangaliwa upya, ila ametaka watumia hekima na busara kulitafakari suala hilo .

Pili, Rais Kikwete amewataka wabunge kutumia mkutano wa sasa wa Bunge kulizungumza upya suala hilo .

Hapo, Rais anawatega wabunge, na hasa wa chama chake ambao ‘wametema mate chini’ kuhakikisha posho mpya zinalipwa. Anawataka “wawe makini” kutekeleza lililoko ndani ya uwezo wake kufuta au kubariki.

Posho hizi zinazoleta balaa, zilianzishwa mwaka 2008 na serikali yenyewe na bila shaka rais anao uwezo wa kuziondoa akitaka; badala ya kuwarushia mpira wabunge au kuwaacha wazidi kukabana na Spika wao.

Sheria ya Utawala wa Bunge (National Assembly Administration Act) ya mwaka 2008, kifungu cha 19(d), kinataja posho za aina tatu – usafiri, kujikimu na wasaidizi zinazoweza kutolewa kwa wabunge kama rais ataeleza kwa maandishi.

Katika orodha hiyo, hakuna posho ya vikao.

Hata hivyo, kifungu cha 19(d) (iv) kimempa mamlaka rais kutoa posho nyingine kwa wabunge kwa kadri atakavyoelekeza.

Kifungu hiki kimetoa mwanya wa kutolewa kwa waraka wa Katibu Mkuu Kiongozi Ofisi ya Rais 25 Oktoba 2010 wenye Kumb. Na. CAB111/338/01/83 wa Masharti ya Kazi ya Mbunge unaoeleza viwango vya posho mbalimbali, ikiwemo posho hii mpya.

Kwa hiyo, pamoja na posho ya vikao kutotajwa kwenye sheria, Ofisi ya Rais (Ikulu) iliamua kuiongeza siku chache kabla ya uchaguzi mkuu uliopita. Na ndiyo posho inayochanganya wananchi.

Katibu wa Kamati ya Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, katika taarifa yake maalum kuhusu suala hili, anasema kamati yao inataka posho hiyo ifutwe mara moja kama sehemu ya mchakato wa kubadili mfumo mzima wa malipo ya posho kwa watumishi wa umma.

“Badala ya Rais Kikwete kukwepa wajibu huo wa kisheria na kuhamisha mzigo kwa wabunge, anapaswa yeye mwenyewe kufanya uamuzi wa kukataa nyongeza ya posho za vikao na kufuta posho hizo katika mfumo mzima wa utumishi wa umma,” anasema.

Mnyika ambaye ni mbunge wa Ubungo, anasema posho hizo hazizingatii uwezo wa serikali ambayo inakiri uchumi unasuasua.

Kwa sasa, serikali ina tatizo kubwa la fedha; moja ya sababu ikiwa ni kupungua kwa mchango wa wahisani. Serikali inakopa ili kuziba pengo la kibajeti liliopo.

Wakati wabunge wa CHADEMA wana msimamo huo, wenzao wa CCM wameendelea kupambana na serikali wakitaka ilipe posho hizo mpya kwa madai kuwa gharama za maisha zimezidi kupanda huku wengi wakikabiliwa na madeni.

Lakini CCM, chama chao, kupitia Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kimepingana nao kikitaka watumie busara, wafungue masikio kusikiliza sauti ya Watanzania waliowachagua ikiwezekana waachane nalo.

“CCM inaupongeza na kuunga mkono msimamo wa Rais Kikwete kama ulivyonukuliwa na taarifa ya Ikulu kuwa ni vizuri wabunge wakalitafakari upya suala hili kwa maslahi mapana ya waliowapa dhamana ya kuwawakilisha bungeni,” amesema.

Hata hivyo, kauli ya CCM inaelezwa na Mnyika kuwa ni ya kinafiki, isiyoonyesha uongozi thabiti na inayolenga kuihami CCM na hasira ya umma dhidi ya viongozi waandamizi wa chama tawala na wabunge wake kutaka nyongeza ya posho za vikao kinyemela.

Mnyika anasema kauli ya CCM kumpongeza Rais Kikwete, ambaye pia ni mwenyekiti wake kwa kutupa mzigo kwa wabunge katika suala ambalo kisheria ni lake kuliamua , ni ishara ya CCM kulea misingi ya kutowajibika miongoni mwa viongozi wakuu wa serikali na chama hicho.

“Iwapo CCM ingekuwa na dhamira ya kweli ya kukataa posho za vikao ingefanya maamuzi ya kukataa kupitia vikao vya chama hicho vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, vilivyoongozwa na mwenyekiti wa chama hicho.”

CCM ingeitumia vizuri kete hii muhimu, ingepata hadhi hasa kwa kuwa jambo hilo lilishakataliwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano uliopitishwa na Bunge mwaka 2011.

Ifike hatua sasa kupima utendaji wa vyama vya siasa kwa maslahi ya umma badala ya propaganda zinazoenezwa kama sababu za kupandisha posho za kukaa – na kusinzia kama wanavyokutwa baadhi ya wabunge.

Fedha zinazotakiwa kulipa wabunge zitumike kuongeza  mishahara kwa watumishi wa umma kwa kuzingatia ujuzi, nafasi na wajibu ili walipwe kwa haki kwa kile wanachofanya.

0
No votes yet