Ziko wapi Sh. 55.4 bilioni?


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 02 March 2011

Printer-friendly version

SERIKALI haina risiti kuthibitisha kupokea zaidi ya Sh. 55 bilioni kutoka kwa makampuni ya madini nchini, MwanaHALISI limebaini.

Kawaida serikali ikilipwa, sharti itoe risiti ya kupokea fedha; lakini hakuna kumbukumbu za kutosheleza maelezo kuwa serikali imepokea kiasi kinachodaiwa kutolewa na makampini.

Kwa mfano, hakuna risiti zinazoonyesha serikali ilipokea zaidi ya Sh. 58.4 bilioni ambazo ni sehemu ya fedha zilizolipwa na makampuni ya madini kati ya 1 Julai 2008 na 30 Juni 2009.

Kiwango hicho ni sawa na asilimia 5.4 ya kiasi cha shilingi trilioni moja (Sh. 1 trilioni) ambacho Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, aliwahi kutamka kuwa serikali inapata kwa mwaka katika sekta hiyo.

Uchunguzi huu umo katika Ripoti ya Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji (Tanzania Extractive Industry Transparency Initiative – TEITI) ya 2008/2009 iliyowekwa wazi jijini Dar es Salaam, 11 Februari mwaka huu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina haikuambulia “hata senti tano” kutoka kwenye makampuni ya madini ambako ina hisa na ingetakiwa kupata gawio.

Ripoti imeshughulikia migodi ya Mererani (tanzanite), Buzwagi, Tulawaka, North Mara na Resolute (dhahabu); Williamson Diamond na El Hillal (almasi).

Serikali ina hisa katika makampuni ya Williamson Diamond inayochimba almasi, Mwadui mkoani Shinyanga na Pan African Energy Tanzania inayochimba gesi Songosongo katika eneo la Mnazi Bay mkoani Mtwara.

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kupimwa katika sekta ya madini kwa vigezo vya uwazi na uwajibikaji. Ripoti hii imetoa picha ya sababu zinazolifanya taifa lisinufaike kwa utajiri mkubwa wa rasilimali zake.

Chini ya utaratibu huo wa EITI, serikali za nchi zilizokubali kupimwa kwa vigezo vya uwazi na uwajibikaji, hutakiwa kuweka wazi mapato zilizokusanya kutoka katika makampuni yanayovuna maliasili kutoka katika nchi hizo huku makampuni nayo yakitakiwa kuweka wazi malipo yote yaliyofanya kwa serikali.

Ni kwa kulinganisha kiasi kilichoonyeshwa kutolewa na makampuni ya madini na kile kilichotangazwa na serikali, TEITI imeweza kubaini upungufu wa kutokuwepo uthibitisho wa kupokea Sh. 55 bilioni katika mwaka mmoja tu.

Hata hivyo, kampuni ya uhasibu Hart Nurse ya Uingereza iliyoandaa takwimu hizi imesema bado serikali ya Tanzania inafanya shughuli zake kwa mkono, bila kompyuta, jambo ambalo imesema linaweza kuchangia kutopatikana takwimu sahihi.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, makampuni yalitoa taarifa ya kuonyesha yalilipa kiasi cha dola za Marekani 84.4 (Sh. 127 bilioni) lakini serikali ilionyesha kuwa imepokea kiasi cha dola 48.3 (Sh. 72.4 bilioni), na hivyo kukiwa na ‘upotevu’ wa dola 36.5 (Sh. bilioni 55).

Ripoti hiyo haikutoa ufafanuzi kuhusu malipo hayo lakini Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Kiraia ya forDIA, Buberwa Kaiza, alisema fedha hizo, Sh. bilioni 55, inahusisha kodi na mrabaha ambazo makampuni hayo hulipa kwa serikali.

Buberwa ambaye pia ni miongoni mwa wajumbe wa bodi ya EITI hapa nchini, alilithibitishia MwanaHALISI kuwa katika hizo Sh. 55 bilioni, mrabaha ni dola 17.05 milioni (Sh. 25.6 bilioni) na zilizobakia ni kodi za aina nyingine kama vile ya mapato.

“Baada ya kutoka kwa ripoti hii, sasa litakuwa ni jukumu la bodi ya kimataifa ya EITI kupitia na kuona kama wana cha kusema.

“Wakiona Tanzania inafaa kuwa mwanachama kamili wa EITI tutakwenda kuwaeleza wananchi kilichopo ndani yah ii ripoti na kutaka maelezo. Kama ripoti itasema hatufai, basi tutaanza moja tena kuangalia wapi tulikosea kwenye ripoti hii,” alisema.

Mambo mengine yaliyoibuka katika ripoti hiyo ni pamoja na hatua ya makampuni ya madini nchini kupeleka ripoti yakidai kuwa makato ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa wafanyakazi wake, ni sehemu ya mapato ya serikali.

Ripoti inasema jambo hilo si sahihi, kwa vile makato hayo, japo huchukuliwa na serikali, hayahesabiki kama mapato kwa vile kimsingi ni stahili za wafanyakazi.

Lakini ingawa makampuni yanajua hilo, yalifanya hivyo ili kuongeza ukubwa wa mapato ya serikali kwenye sekta hiyo, imeelezwa.

Kuna aina mbalimbali za kodi ambazo makampuni ya madini yanayofanya kazi nchini hutakiwa kulipa serikalini lakini NSSF si miongoni mwa kodi hizo.

Malipo husika ni yale ya mapato (ya kampuni na yale yatokanayo na mishahara ya wafanyakazi), ushuru wa forodha kwa bidhaa kama vile magari na vipuri vya mashine, mrabaha (asilimia tatu kwa dhahabu, tano kwa almasi na 12.5 kwa gesi) na ushuru wa vitu kama magari.

Ripoti ya TEITI imeonyesha pia namna makampuni ya kuchimba madini yalivyodai kwamba yametumia mabilioni ya shilingi kulipa kodi zilizotokana na uagizaji wa mafuta kutoka nje, wakati makampuni hayo yana misamaha ya kodi kwenye eneo hilohilo.

Kwa mujibu wa utaratibu uliopo, makampuni hayo huagiza mafuta kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kufanya shughuli zao na kuyalipia kodi kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) lakini serikali huwarejeshea fedha hizo.

Hata hivyo, kampuni hiyo ya uhasibu iliyofanya ukaguzi, ilibaini kuwa makampuni hayo yaliwasilisha taarifa za malipo hayo bila ya kueleza kuwa fedha hizo hurejeshwa kwao.

Maana ya maelezo ya ripoti hii mpya ya TEITI ni kuwa katika miaka ya nyuma, mapato ambayo makampuni haya yalikuwa yametangaza kuwa yameingiza kwa serikali kupitia shughuli zao yalikuwa na “mushkeli.”

Ripoti hiyo imegundua kuwa kampuni ya El Hillal inayochimba almasi jirani na mgodi wa Mwadui mkoani Shinyanga, haijapeleka malipo yoyote kwa serikali katika kipindi kinachoripotiwa na TEITI.

“Wakati sisi tulitaka kutazama hesabu za kampuni hiyo katika kipindi cha Julai 2008 hadi Juni 2009, kampuni hiyo ilituletea hesabu za mwaka 2009 ambao sisi hatukuwa na shida nazo,” inasema ripoti hiyo.

Kwenye ofisi ya msajili ya hazina hakukuwapo taarifa zozote za malipo yaliyofanywa na kampuni pamoja na ile ya Williamson Diamond ambako serikali ina hisa kiasi cha asilimia 25.

Kampuni hiyo ya Williamson imelipa karibu kodi zote nyingine ilizotakiwa kulipa, lakini hakuna taarifa zozote za kupeleka Hazina gawio la serikali kama ilivyo taratibu.

Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, Tanzania kwa sasa ni ya nne kwa uzalishaji wa madini ya dhahabu barani Afrika, ikiwa nyuma ya Afrika Kusini, Ghana na Mali.

Mpango wa Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji (EITI) ni mpango wa kimataifa wenye lengo la kuhakikisha kuwa nchi zilizojaaliwa utajiri wa maliasili zinafaidika na mali hizo.

Tanzania ilikubali rasmi kuwa mwanachama wa EITI Novemba 18 mwaka 2009, na kwa sasa ni miongoni mwa nchi 28 duniani zinazotafuta nafasi ya kuwa mwanachama kamili wa EITI.

Kwa sasa ni nchi tano tu duniani –Azerbaijan, Ghana, Mongolia, Liberia na Timor ya Mashariki ndizo zilizotimiza vigezo vya kuwa wanachama kamili wa EITI.

Kwa sasa, Jaji Mark Bomani ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya EITI nchini, inayoundwa na wawakilishi 15 kutoka serikalini, makampuni ya madini na asasi za kiraia ambazo zote zina wajumbe watano kila moja.

MwanaHALISI limekokotoa hesabu za makala hii kwa kiwango cha dola moja ya Marekani sawa na Sh. 1600.

0
No votes yet