Zilizokuwa changamoto 2005 ni matatizo leo Zanzibar


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 21 January 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

Katika safu hii adhimu, Mwandishi ameanza kudodosa hali ya mambo ilivyokuwa wakati wa uchaguzi mkuu wa 2005 na kujaribu kuangalia hali ilivyo leo visiwani Zanzibar. Fuatilia muendelezo wa makala zake zinazokupa hali ya mambo upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano.

HATA mvuvi wa Zanzibar anakabiliwa na maisha ya kifukara kama mfanyakazi wa serikali na mkulima. Anavua kwa zana duni licha ya kuwepo mradi mkubwa wa Usimamizi wa Bahari na Mazingira ya Ukanda wa Pwani (MACEMP).

Mkazo wa mradi huu ni uanzishaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kuongezea kipato wavuvi – hii ni miradi mbadala ya kazi ya uvuvi – na kwa sehemu kubwa ni kuhimiza uvuvi endelevu unaosaidia kuimarisha mazingira ya baharini na kudhibiti uharibifu wa matumbawe ambamo ndimo yalimo mazalio ya samaki.

Malalamiko mengi yamekuja kwamba wakati wavuvi wanazuiwa kutumia nyavu za macho madogo na uvuvi wa madema, wanapata msaada mdogo kutokana na mradi huo unaofadhiliwa kwa nguvu ya mkopo wa Sh. 3 bilioni zilizotolewa na Benki ya Dunia.

Wakati wavuvi wanalalamika, serikali inaendelea kutoa vibali kwa meli za kigeni ambazo wavuvi wake hutumia zana za kisasa kuvulia samaki kwenye bahari kuu ambako katu wavuvi wenyeji hawafiki. Raslimali kubwa ya samaki inasafirishwa nje ya nchi na ni chache zilizoajiri wafanyakazi wazalendo.

Samaki anaopata mvuvi wa Zanzibar, hawatoshi kupata fedha za kununulia mahitaji yake ya lazima kwa siku mbili. Ndio kusema mvuvi huyu lazima aingie baharini kila siku ili kuendelea kupata chakula cha familia yake.

Akiumwa, wavuvi wenzake wanaoshirikiana chombo cha kuvulia, wanaweza kumsaidia kupata matumizi kwa siku chache mno. Akiendelea kuugua, huo ni mtihani mkubwa kwake. Wala wenzake hawalaumiki, tatizo lao ni kwamba wanachokipata kwa siku hakitoshelezi mahitaji yao.

Umasikini. Uliopo Unguja na Pemba ni wa kutupwa na ni chimbuko la vijana wanaomaliza elimu ya lazima – darasa la kwanza hadi kidato cha pili – kukimbia vijiji na kuhamia mjini kwa matumaini ya kupata kazi ya mshahara. Wengi hawa huishia kuuza chipsi na kuwa tingo wa daladala au magari ya mizigo. Lakini wasiobahatika, hubaki vijiweni kupiga soga na kuhamasika na shughuli ya mapenzi wakiwa wadogo.

Zanzibar ina raslimali ya kutosha ya baharini na fukwe zake ambako sekta ya utalii inazidi kuwa tegemeo kubwa kwa pato la taifa. Tatizo linalokua ni kwamba vijana wenyeji hawana ujuzi wa kufanya kazi katika sekta ya utalii na serikali haina mchango wa maana kuwasaidia.

Katikati ya mwezi uliopita, nilimsikia Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, mwanasiasa kijana aliyetumainiwa kubadilisha hali za vijana kiajira, anarudia mbiu niliyopata kuisikia miaka saba iliyopita:

“Tutahakikisha vijana wa Unguja na Pemba wananufaika na raslimali inayokuza sekta ya utalii.”

Mwaka 1992, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) lilisaidia SMZ kujenga Chuo cha Utalii Maruhubi kwa lengo la kusaidia elimu ya kuhudumia watalii miongoni mwa vijana wa Zanzibar.

Leo wanaoingia chuo hicho ni wenye fedha tu na kwa kuwa ni sehemu ndogo mno kwa wenyeji, faida inakwenda kwa vijana watokao nje ya Zanzibar – hasahasa nchi za Afrika Mashariki; Tanzania Bara, Burundi na Kenya. Somalia inatajwa kuingiza watu wengi kwenye sekta hiyo.

Kijana maarufu anayeitwa Zenj Freedom kupitia mtandao wa Zanzinet, aliwahi kunieleza tatizo la mamia ya vijana wenzake kushindwa kujiunga na chuo hicho kwa sababu hawana uwezo wa kulipia mafunzo yanayotolewa kutokana na ufukara unaokabili familia zao.

Serikali haina mikopo kwa vijana labda wale wanaotoka familia za wana wa Afro-Shirazi Party (ASP) na watoto wa mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu, wakurugenzi na makamishna katika wizara, idara na mashirika ya serikali. Wengine ni watoto wa makada wa CCM waliotumika kusaidia mikakati ya kupindua matokeo ya uchaguzi tangu mwaka 2000 kwa jina la Janjaweed.

Na vijana hao ambao wengi wao hawakufikia sekondari ndio wanaoingizwa kwenye ajira ya serikali. Hakuna anayejali matokeo ya utafiti wa kisayansi uliobaini kwamba zaidi ya asilimia 80 ya watumishi wa SMZ hawana sifa walimoajiriwa. Utafiti huo ulifanywa mwaka 2005 na wataalamu wa Uingereza.

Kwa sababu hawana elimu ya kutosha kushindana katika soko la ajira, na kwa sababu wanatoka katika familia fukara, maelfu ya vijana wa Zanzibar wanabaki nje ya nguvu kazi ambayo ingeweza kusaidia ujenzi wa maendeleo ya nchi yao.

Kilichobaki ni baadhi yao kujishughulisha na kazi za kipato cha kutwa zisizo na mikataba na zilizojaa unyanyasaji na dhulma kwa wafanyakazi. Sehemu nyingine kwa kuona wamekata tamaa na matumaini ya maisha mazuri, wanabaki mitaani na hatimaye kugeuka watumiaji wa madawa ya kulevya.

Hapo kinachotokea ni kuchangia uambukizaji virusi vya ukimwi, tatizo kubwa miongoni mwa vijana wa Zanzibar hasa wakati huu wakichanganyika na athari za kuporomoka kwa utamaduni na mila za Kizanzibari kulikosababishwa na uingiaji usiodhibitiwa wa wageni ulioanza tangu kuondolewa kwa utaratibu wa matumizi ya pasi za kusafiria kwa mtu anayeingia na kutoka Zanzibar.

Uchaguzi imekuwa chimbuko kubwa la uingiaji holela wa wageni visiwani. Hakuna takwimu sahihi lakini wapo wanaosema wageni wapatao 150,000 wameingia Zanzibar kwa sababu ya uchaguzi tangu mwaka 1995. Chini ya aslimia 50 walirudi walikotoka, wengine walibaki na kuanza maisha mapya.

Tembelea masoko ya Kinyasini, Mkokotoni na Nungwi halafu fika maeneo ya shughuli za kitalii ya Matemwe, Kiwengwa, Michamvi, Paje, Bwejuu, Nungwi na Mji Mkongwe wa Zanzibar. Humu utashuhudia shughuli nyingi za biashara zikiwemo za utoaji huduma kwa watalii zikifanywa na wageni.

Sehemu kubwa ya wageni hao wakiwemo wanawake wanaofanya kazi ya mama ntilie waliogoma kuondoka hata walipotakiwa na waliowaleta ili kurudi mkoani Dar es Salaam, sasa wanatambuliwa kama Wazanzibari baada ya kupatiwa kiulaini kile kiitwacho kitambulisho cha Mzanzibari kilichotolewa kuanzia mwaka 2005 na ambacho kinakwisha muda wake mwakani.

Nimejadili umasikini na ajira kama changamoto. Wiki ijayo, nitajadili sekta ya biashara ilivyoathirika kutokana na sera mbovu za serikali.

0
No votes yet