Zimbabwe haina mnyongaji


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 21 April 2010

Printer-friendly version

SERIKALI ya Zimbabwe imetangaza rasmi kwamba inatafuta kwa hali na mali mtu aliye tayari kufanya kazi ya unyongaji wa wafungwa waliohukumiwa kifo nchini humo.

Tangu mwaka 2005, Zimbabwe imekuwa haina mtu anayefanya kazi ya kunyonga, jambo linaloelezwa kuwapa mateso makali ya kisaikolojia wanaosubiri kunyongwa.

Inaelezwa kwamba mtu aliyekuwa akifanya kazi hiyo hadi mwaka 2005 alikuwa na asili ya Malawi na aliondoka mara tu baada ya kufanikisha unyongaji wa majambazi wawili maarufu nchini humo.

Mmoja wa maofisa wa ngazi za juu wa Idara ya Magereza ya Zimbabwe, Owen Chinamasa, amesema raia huyo wa Malawi aliamua mwenyewe kuacha kazi.

“Kazi ya kunyonga ina mambo yake. Kazi yenyewe haiishii kwenye kitendo chenyewe. Inahusu pia ni namna gani mnyongaji anajisikia baada ya kumaliza kazi hiyo,” alisema.

Ofisa huyo alisema serikali ilikuwa na taarifa kwamba mnyongaji huyo alikuwa na tabia ya kujilaumu sana mara baada ya kumaliza kunyonga, jambo ambalo halitakiwi kwa anayefanya kazi hiyo.

“Kazi ya kunyonga si kwa watu wenye mioyo myepesi. Kazi hii inataka ujasiri wa aina yake. Kama wewe una moyo wenye kujutia matendo yako, hii si kazi yenye kukufaa,” alisema.

Taarifa kutoka idara hiyo ya magereza inasema kwamba kwa sasa kuna zaidi ya wafungwa 50 wanaosubiri kunyongwa katika magereza mbalimbali nchini Zimbabwe.

Miongoni mwao, yupo Shepherd Masango aliyehukumiwa adhabu hiyo miaka 13 iliyopita, lakini hadi sasa bado hajanyongwa.

“Kwa kweli nina maisha magumu sana. Nimehukumiwa kifo miaka 13 iliyopita na hadi leo ninaishi lakini sijui hatma yangu. Ninapata mateso makubwa sana ya kisaikolojia,” alisema.

Inadaiwa kwamba wafungwa takribani 12 wamepeleka maombi yao kwa Rais Robert Mugabe kutaka adhabu zao zibatilishwe kutoka kifo kuwa kifungo cha maisha.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya Ikulu ya Zimbabwe zinadai kwamba Mugabe amekataa maombi hayo ya wafungwa kutaka wabatilishiwe adhabu.

Wafungwa hao wamedai kwamba kwa mujibu wa sheria nyingine za Zimbabwe, ikiwamo ile ya masuala ya haki za binadamu, wanachofanyiwa sasa ni kinyume cha ubinadamu.

Kwamba adhabu ya kifo inatakiwa itekelezwe haraka mara tu baada ya hukumu na si miaka mingi kama ilivyo kwa wafungwa kama Masango.

Miongoni mwa wafungwa waliomwandikia barua Mugabe kumwomba awabatilishie adhabu ni Mantashe Zvikomborero, aliyehukumiwa kifo mwaka 2005.

“Kila ninapomuona mtu kama Mashonda huwa ninaishiwa na nguvu. Tayari nina miaka mitano jela na ninapofikiria uwezekano wa kukaa mwaka mwingine zaidi katika hali hii najisikia vibaya mno,” alisema Zvikomborero.

Zimbabwe ni miongoni mwa nchi za kiafrika ambazo bado zinaendeleza adhabu ya kifo na inasadikiwa watu 65 wamenyongwa tangu nchi hiyo ijipatie uhuru mwaka 1980.

Wafungwa wanaosubiri kunyongwa nchini Zimbabwe wamewekwa katika gereza lenye ulinzi mkali la Chikurubi lililopo Kilometa 20 kutoka mji mkuu Harare.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa la kutafuta mnyongaji, anahitajika mtu mwenye elimu ya sekondari na hakuna uzoefu wa aina yoyote unaohitajika.

Kazi ya unyongaji ina tofauti kubwa na kazi nyingine. Kuna siku chache ambazo anaweza kupata kazi ya kunyonga watu watatu hadi wanne.

Lakini kwa kipindi kirefu, mnyongaji anaweza kukaa kwa zaidi ya miezi au mwaka mzima bila ya kunyonga mtu na bado akaendelea kupokea mshahara wake kama kawaida.

Mtu aliyekuwa akifanya kazi ya kunyonga nchini Zimbabwe hafahamiki kwa sura wala jina na kazi ya mnyongaji kwa kawaida huzungukwa na usiri mkubwa ili kulinda usalama wake.

Ingawa serikali imesema uzoefu wa kufanya kazi hiyo si jambo la muhimu, kuna mambo ya msingi ambayo mnyongaji ni lazima ayafahamu.

Kwanza Zimbabwe inatumia mfumo wa kizamani wa kunyonga kwa kutumia kamba. Maana yake ni kuwa, mnyongaji anatakiwa kufundishwa jinsi ya kuifunga kamba ya kunyongea.

Zaidi ya hapo, mnyongaji anatakiwa kufahamu kuhusu namna ya kumsimamisha mtu anayepaswa kunyongwa, ni wakati gani atakuwa amekufa na kuiandaa maiti kabla haijachukuliwa.

Ndiyo maana, Chinamasa anafikiri kwamba kazi ya mnyongaji si yenye kuweza kufanywa na kila mtu. Ni kwa ajili ya wale wenye roho za chuma.

Baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu wamedai kuwa kazi ya kunyonga ni ya kinyama na hakuna mwanadamu anayestahili kuifanya.

Kwa mujibu wa mwanaharakati kutoka Zambia, Enock Chota, badala ya serikali ya Zimbabwe kuhangaika kutafuta mnyongaji, ni heri ikaamua kuachana na sheria ya kunyonga moja kwa moja.

“Kama wangekuwa wameachana na sheria hii ya kunyonga, leo hii suala hili la kutafuta mnyongaji lingekuwa halipo. Mnalipaje mshahara mtu ambaye kazi yake ni kuua?” Alihoji.

Chama cha Movement for Democratic Change (MDC), kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai, kinafahamika kwamba kinapinga adhabu ya kunyonga.

MDC imeingia kwenye serikali ya umoja wa kitaifa na Mugabe na zipo taarifa kwamba kwenye muswada wa mabadiliko ya katiba ya Zimbabwe, suala hili la adhabu ya kifo litaguswa.

Lakini, kwa kipindi hiki kabla mabadiliko hayo ya katiba hayajafanyika, kazi ya kuendelea kutafuta mnyongaji inaendelea.

0
No votes yet