Zitto ahusishwa na Rostam


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 15 December 2010

Printer-friendly version
ZITTO Kabwe, Naibu katibu mkuu wa CHADEMA

ZITTO Kabwe, naibu katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amekuwa na mawasiliano ya karibu na na mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, imefahamika.

Kufichuka kwa taarifa za mawasiliano kati ya Zitto na Rostam kumekuja wiki moja baada ya gazeti hili kuchapisha mawasiliano kati ya Zitto na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa nchini (TISS), Jack Zoka.

Aidha, kufichuka kwa mawasiliano kati ya Zitto na Rostam kumekuja siku mbili baada ya mama mzazi wa Zitto, Shida Salum kunukuliwa akisema, “Mwanangu ni mkorofi.”

Mama Zitto alikieleza kikao cha Kamati Kuu (CC) ya chama chake kilichofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, “Namfahamu mwanangu. Ni mkorofi. Si msikivu.”

Kwa mujibu wa rekodi ya mwingiliano wa simu za mdomo na maandishi (sms) kutoka kwa Zitto kwenda kwa baadhi ya vigogo wa ngazi ya juu serikalini, TISS na Rostam, watu hao wawili wamekuwa wakijadiliana mambo kadhaa.

Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakijadiliwa na viongozi hao, yanahusu CHADEMA, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na taifa kwa ujumla.

Rostam ambaye CHADEMA imekuwa ikimtuhumu kuhusika katika kashfa mbalimbali za ufisadi, ni mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CCM.

Gazeti hili limeshindwa kujua mapenzi ya Rostam kwa CHADEMA hadi kujipa jukumu la kujadiliana na Zitto juu ya “uhai bora” wa chama hicho.

Kwa mfano, Zitto na Rostam walifanya mawasiliano ya simu mara tano hapo tarehe 11 Agosti 2010. Simu iliyotumika katika mawasilino hayo, ni Na. +255756809535 ambayo hutumiwa na Zitto na +255754555555 ambayo hutumiwa na Rostam.

Mawasiliano hayo yalifanyika saa 07:08:35, saa 22:09:02, saa 22: 28: 39, saa 22:49:54, saa 22:44:37 na saa 22:45:09.

Wakati mawasiliano hayo yanafanyika simu ya Zitto ilikuwa inasomeka kuwa yuko Uzunguni, Dodoma, huku simu ya Rostam ikisomeka kuwa ilikuwa Area D, Dodoma.

Mawasiliano mengine yalikuwa katika maeneo tofauti. Mathalani mawasiliano ya Zitto na Rostam yalyofanyika 30 Novemba 2010 yalionyesha kuwa Zitto yuko Ohio, Ilala, Dar es Salaam. Yalifanyika saa 14:58:42, saa :16:41:58, saa 15:38:00, saa 16:09:56 na 17:48: 35.

Mawasiliano mengine ya Zitto na Rostam yalifanyika siku mbili kabla ya wabunge wa CHADEMA hawajakutana Bagamoyo.

Mawasiliano hayo yalifanyika tarehe 7 Desemba 2010 saa 07: 57:27, saa 14:32:08, saa 09:44:36 na saa 14:07:07.

Haijaweza kufahamika pia kiini cha mawasiliano kati ya Zitto, Zoka, Rostam na vigogo wengine wa serikali, CCM na usalama wa taifa.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa wetu kutoka ndani ya kikao cha CHADEMA, awali mama Zitto alieleza masikitiko yake kuhusiana na taarifa mbalimbali zinazomhusu mwanawe.

“Najua mwanangu ni mkorofi. Lakini kuna njia ya kufanya kuliko kukitia chama msukosuko…Kila mara Zitto, Zitto, Zitto.  Haya mambo hayana faida kwa chama,” alieleza.

Hata hivyo, vyanzo huru vya taarifa vimeeleza MwanaHALISI kuwa mpango uliopo ni kumtumia Zitto “kusambaratisha CHADEMA.”

“Kaka, nakuhakikishia kuwa upo ushahidi wa kutosha kwamba Zitto anatumika kuvuruga CHADEMA. Kuna baadhi ya vigogo ndani ya CCM na serikali, wanaomtia ujinga kwa kumueleza, ‘kwa hali ilivyo ndani ya CCM, wapo baadhi ya watu  wanatamani kuondoka. Lakini hawawezi kwenda CHADEMA kwa sababu kinaongozwa na Mbowe (Freeman Mbowe),’” ameeleza mtoa taarifa.

Anasema, “Hivyo wanampampu Zitto kugombea uenyekiti. Wanataka Mbowe ang’oke na CHADEMA kisambaratike. Ni kwa sababu, wote wanaomtumia Zitto, wanajua kuwa huyu bwana mdogo hana uwezo wa kuongoza CHADEMA na haaminiki.”

Akiongea kwa kujiamini, mtoa taarifa anasema, “Ni mbinu zilezile zilizotumiwa NCCR- Mageuzi, ambapo baadhi ya vigogo  wa idara ya usalama wa taifa walitumia fedha ili kumng’oa Marando (Mabere Marando), katika uongozi wa chama.”

Anasema taarifa kwamba wapo watu wanataka kuondoka ndani ya CCM na kujiunga na CHADEMA ni mkakati unaosukwa kwa ustadi mkubwa na baadhi ya vigogo wa serikali kwa kushirikiana na  usalama wa taifa.

Inadaiwa ni katika mkakati huo, ndimo linapatikana jina la Rostam ambaye  uongozi wa juu wa chama hicho umekuwa ukimtuhumu kuhusika katika kashfa mbalimbali za ufisadi nchini.

“Unajua ndugu yangu hapa Tanganyika, Rostam angependa sana awe na uwezo wa ku-control vyama vyote vinavyokua, hasa CHADEMA kwa sasa; ingawa uwezo wake wa kupenyeza unakuwa mgumu.

“Mkakati wake ni kumweka mtu wao katika uongozi wa juu wa CHADEMA ili waweze kumuendesha. Mpango huo ukifanikiwa, kina RA (Rostam) wataacha ugomvi na CHADEMA. Kwa sasa mtu wao ni Zitto. Na kuna mambo mengi ya siri ambayo RA amekubaliana na Zitto,” anaeleza mtoa taarifa mmoja ambaye yuko karibu na Rostam na Zitto.

Mjadala juu ya mwenendo wa mashaka wa maisha ya kisiasa ya Zitto, uliibuka baada ya katibu wa wabunge wa CHADEMA, John Mnyika kuwasilisha taarifa ya shughuli za kamati hiyo mbele ya Kamati Kuu.

Kikubwa kilichojadiliwa ni hatua ya Zitto kuongoza kikundi cha baadhi ya wabunge kusaliti maamuzi halali ya kamati ya wabunge wa chama hicho.

Zitto anatuhumiwa na wabunge wenzake kutotii agizo la kutoka nje wakati Rais Jakaya Kikwete anahutubia Bunge, 18 Novemba 2010.

Katika taarifa yake kwa CC, Mnyika alisema katika kushughulikia suala hilo, hakukuwa na lolote la kuviziana kama ambavyo baadhi ya wajumbe wamedai.

“Hakuna kanuni iliyovunjwa, wala hakuna kinachoitwa kuviziana. Wabunge walikuwa na hasira sana juu ya hatua ya Zitto na wenzake kutotii agizo la kamati na kupita katika vyombo vya habari kupotosha ukweli,” alisema Mnyika kwa sauti ya upole.

Akiongea kwa sauti ya kusisitiza, Mnyika alisema, “Mheshimiwa mwenyekiti, kwa kweli, wabunge walitaka hata kuwapiga wabunge walioasi makubaliano yao. Uongozi wa Kambi ukafanya juhudi kulipeleka mbele suala hili, angalau kupunguza munkari wa wabunge,” alieleza.

Ni katika kikao hicho cha wabunge kilichofanyika Bagamoyo, ndipo wabunge walipiga kura ya kutokuwa na imani na Zitto.

Kile kilichoitwa, “kuviziana” kiliibuliwa ndani ya kikao cha CC na Dk. Kitila Mkumbo, ambaye amenukuliwa akisema ameshutushwa na hatua ya wabunge kumhukumu Zitto wakati ni mgonjwa.

Alikuwa ni Benson Kigaila, mjumbe wa CC aliyeeleza viongozi wenzake umuhimu wa kujenga chama imara badala ya kuangalia mtu.

“Mtu aliyekosea, lazima aadhibiwe. Tusiangaliea kama ataanguka, au atanufaika. Kwa muda mrefu, chama hiki kimenufaika kwa makosa ya CCM, ambapo kutokana na makundi yanayokinzana, wameendelea kukumbatia maovu. Ni lazima chama kichukue hatua za kukabiliana na magenge haya,” alieleza.

Mjumbe mwingine wa CC aliyeongea kwa sharti la kutotajwa gazetini, ameliambia gazeti hili, “Yale mambo yalikuja kama taarifa, si vingenevyo. Jukumu sasa, liko kwa Zitto mwenyewe kujipima kama anaweza kuongoza watu ambao hawana imani naye.”

Baada ya kupeleka taarifa hiyo CC, wabunge wameeleza, “…Tunapeleka maamuzi yetu haya kwa Zitto. Anatakiwa kuamua ama kuachia ngazi au kusubiri hatua nyingine zinazofaa kuchukuliwa kwa mtu kama yeye katika kikao chetu kingine.”

Mara baada ya mjadala wa Zitto kwa CC kutoingilia maamuzi ya Kamati ya wabunge wake, ndipo uamuzi wa kuunda kamati ndogo ya “kumpa ushauri” Zitto ilipoundwa.

Kamati hiyo inaongozwa na Profesa Mwesiga Baregu.Wajumbe wake ni Nyangali Shilungushela, SylivesterMasinde na Mama Zitto.

Kazi ya kamati ya Baregu ni kufuatilia nyendo za Zitto, kumshauri jinsi ya kujibadilisha ili hatimaye arejee katika njia iliyonyooka.

0
Your rating: None Average: 5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: