Zitto na akili ya Andy Capp


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 01 December 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala
Andy Capp

RAFIKI wa karibu, mwandani au mpenzi mkubwa wa Andy Capp, ni pombe aina ya Whisky.

Mahali popote anapokaa Andy Capp, (katuni maarufu katika magazeti ya The Daily Mirror na The Sunday Mirror ya Uingereza), pembeni kuna glasi ya whisky.

Siku moja alikwenda baa akapiga ‘maji’ na wakati anaondoka alinunua mzinga halafu akashika njia kurudi nyumbani.

Alipofika nyumbani, bahati mbaya, aliteleza akaanguka kwenye kizingiti akachubuka mkononi. Baada ya dakika kadhaa, alijizoazoa, akainuka.

Andy aliona majimaji chini. Akili yake ikamtuma kuwa chupa ya whisky ilikuwa imepasuka, akadhani majimaji aliyokuwa anayaona yalikuwa whisky.

Alikasirika. Lakini alipochovya kidole kwenye majimaji yale na kukilamba, alishukuru kubaini kwamba kumbe ilikuwa damu.

Andy Capp alitabasamu akisema, “nilidhani whisiky”. Alipoingia ndani alikaa kwenye kochi akaendelea kupiga maji huku damu ikimchiriziki bila kuhofia madhara.

Andy Capp ni mlevi wa pombe, lakini wapo walevi wa sifa ambao nao huwa hawafikirii madhara ya ulevi wao.

Walevi wa sifa hutembea mabega juu, hubinua midomo kwa kejeli, hudharau hata viongozi wao na hujiona bora.

Naibu katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, amejifikisha hapo. Amelewa sifa za kuitwa mbunge maarufu kijana na mbunge anayeongoza kwa kulichachafya Bunge.

Sasa anaona wengine wote hawafai—na mtu akifuatilia mwelekeo wake, anataka kutembea juu ya mabega ya viongozi wake hasa Mwenyekiti, Freeman Mbowe.

Mlevi wa sifa, kama ilivyo kwa mlevi wa pombe hawezi kuona kosa analofanya. CHADEMA imekua na inahimili mtikisiko wa demokrasia, lakini kinachofanywa sasa na Zitto ni kuingiza uvundo wa sifa kwenye chama.

Zitto anatembea kwenye mstari wake nje ya uliochorwa na chama na hasa maamuzi yanayotamkwa kutoka kinywa cha mwenyekiti wake.

Zitto, mtu aliyetembea nchi nyingi za nje na ambaye amejifunza mifumo tofauti ya uendeshaji siasa kimataifa, anaingiza demokrasia ambayo haivumiliwi na nchi yoyote hata Marekani.

Jenerali Stanley A McChrystal ambaye alikuwa kamanda wa vikosi vya Marekani nchini Afghanistan alikosoa sera ya ulinzi ya Rais Obama. Haikumchukua muda akatupwa nje na nafasi yake ikachukuliwa na Jenerali David H Petraeus.

Alichukulia kuwa ni usaliti mkubwa kwa vikosi hivyo na kauli zake zilichukuliwa kuwa zinahatarisha usalama wa wanajeshi.

Zitto lazima ajue kwamba hawezi kuwa na msimamo wa kukichafua chama chake akabaki salama. Hata CCM wamefikia hapo kutokana na baadhi ya viongozi walioshindwa hoja kwenye vikao kukimbilia kwenye vyombo vya habari kuchafua wengine.

Kama anataka kuwa salama yaani mtu wa kutoa kauli na misimamo inayokinzana na viongozi wenzake aachie madaraka, awe huru.

Kwa tafsiri yoyote ile Zitto anakuwa kama Andy Capp kujali whisky badala ya damu yake yaani anamwonea huruma Rais Jakaya Kikwete lakini anapuuza maamuzi halali ya mwenyekiti wake.

Hawezi kumdharau mwenyekiti wake akadhani atabaki salama ili kumfurahia mwenyekiti wa wenzake hata kama ni wa chama tawala. Ushawishi anaofanya Zitto, kwa tafsiri rahisi, hakubaliani na madai ya chama chake kwamba kura zimechakachuliwa kumpa ushindi ‘huyo anayejikomba kwake’. Kama hivyo ndivyo, anasubiri nini CHADEMA?

Watanzania watamtaka asimame afafanue jinsi yeye na wafuasi wengine waislamu wanavyobaguliwa ndani ya CHADEMA. Aeleze waislamu wangapi wamenyimwa haki.

Maana kati ya makosa yote kuanzia kutoa siri za chama, kuzusha mambo, kutaka awe juu ya mwenyekiti wake (kiongozi wa upinzani bungeni) akidai ana uzoefu zaidi na ni maarufu, hili la udini haliwezi kufumbiwa macho.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: