Zitto ana maslahi yapi NSSF?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 23 March 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi
ZITTO Kabwe

ZITTO Kabwe, mbunge wa Kigoma Kaskazini, amejiingiza katika kazi isiyomhusu. Sasa ametumbikiza hadi Kamati ya bunge ya kusimamia hesabu za mashirika ya umma (POAC) katika “mradi” wa kutetea Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Kisa: Anataka serikali kumilikisha NSSF mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira kwa kile alichoita, “kulinda fedha za umma.” Anasema shirika hilo ndilo lililotoa mkopo wa dola 7 milioni (karibu Sh. 9.5 bilioni) kwa kampuni ya Kiwira Coal Mines Limited. Hadi sasa fedha hizo hazijarejeshwa.

Kwa wanaofahamu kazi za Kamati za Bunge, kazi ya kushauri serikali kukabidhi Kiwira kwa NSSF, si kazi ya kamati ya Zitto. Vinginevyo, anaifanya kazi hiyo kwa malipo na nje ya shughuli za bunge.

Kwa mujibu wa nyongeza ya nane ya kanuni ya 10 (1) ya Kanuni za Bunge, kazi za kamati za Bunge zinazosimamia fedha za umma ni kama ifuatavyo:

Kushughulikia maeneo yaliyokubuhu wizi wa fedha za umma katika wizara za serikali kama ilivyoelezwa na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kazi nyingine, ni kufuatilia utekelezaji wa “mapendekezo yaliyotolewa na kamati hiyo yenye lengo la kuondoa matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma; kutoa mapendekezo na ushauri kwa wizara za serikali kuhusu matumizi mazuri ya fedha za umma.”

Kwa kuzingatia rejeza hizo, anachokifanya Zitto na wenzake katika kamati, ni tofauti na kinyume cha kazi alizopewa.

Kwanza, Zitto anajua kwamba Kiwira Coal Mine (KCM) ulianzishwa na serikali kwa msaada wa fedha na ufundi kutoka serikali ya Jamhuri ya watu wa China. Uzalishaji umeme katika mgodi huu, ulianza mwaka 1988 ambapo megawati sita (6) ziliingizwa katika gridi ya taifa.

Pili, mwaka 2004, serikali ilianza mchakato wa ubinafsishwaji wa mradi huo chini ya kilichoitwa “mamlaka ya ubinafsishaji ya taifa – PSRC.”

Ni ubinafsishwaji huo wenye utata uliosababisha matatizo lukuki. Pamoja na serikali kutoa fedha kupitia PSRC kulipa wafanyakazi 1,632 wa Kiwira, hadi sasa hakuna aliyelipwa.

Aidha, serikali iliutoa mgodi huu kwa bei ya kutupa. Taarifa zinasema, kazi ya tathimini ilifanywa kwa mara ya kwanza mwaka 1988 ambapo thamani ya mgodi ilionekana kuwa Sh. 4.2 bilioni.

Lakini mwaka mmoja baadaye, taasisi moja ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilifanya tena kazi ya tathimini na kugundua kuwa thamani halisi ya mgodi ni Sh. 7 bilioni.

Hata hivyo, pamoja na tafiti zote mbili kufanyika; fedha za umma na rasilimali za taifa kutumika; serikali iliuuza mgodi huo kwa Sh. 700 milioni tu (!)
Tatu, ni serikali ya rais mstaafu Benjamin Mkapa iliyobinafsisha mgodi huu kwa kuwapa kampuni ya “TanPower Resources Limited.” Ilikuja kufahamika kuwa kampuni hiyo inamilikiwa na watu wenye uhusiano wa kifamilia na Mkapa na aliyekuwa waziri wake wa nishati na madini, Daniel Yona.

Tayari kuna taarifa kuwa Tan Power wameifunga TANESCO kulipa kiasi cha Sh. 300 millioni kama gharama za kuweka mitambo – Capacity Charge – kwa kila mwezi. Mabilioni haya ya fedha, ni nje ya zile zitakazolipwa kununulia umeme. Haya Zitto anayafahamu, lakini hataki kuyajadili.

Nne, shirika la NSSF, ambalo msingi wake mkuu wa mapato ni michango ya mafao ya wafanyakazi, lilitoa fedha bila kuwapo dhamana yoyote ya kuwalinda. Hili linathibitishwa na kauli ya NSSF wenyewe na ile ya Zitto inayosema, “Tunataka mradi huu ukabidhiwe NSSF ili kulinda fedha zake ilizotoa.”

Fedha zilitolewa kwa kazi ya kukarabati mitambo. Mkopo huo ulitarajiwa kurejeshwa baada ya kipindi cha miezi sita. Hadi tarehe 20 Machi mwaka huu, hakukuwa na hata shilingi iliyorejeshwa kwa waliokopesha.

Zitto hataki kujadili uhalali wa mkopo uliotolewa na kilichoisukuma NSSF kutoa mkopo. Wala haelezi kama amefanya uchunguzi kujua mradi huu umenufaisha nani.

Mbunge huyu hatafuti mazingira ya mkopo huu: Kama waliotoa mkopo walitishwa au walihongwa. Kama walihongwa, nani alihongwa; kama walitishwa, nani alitishwa na alitishwa na nani.

Hataki tujadili kwa nini NSSF ilikubali kutoa mkopo kwa Kiwira chini ya maelekezo ya serikali, wakati hisa za serikali katika mradi huo, ni asilimia 15 tu; na nani yuko nyuma ya TanPower.

Hakuna mashaka kuwa Kiwira ilinufaisha wamiliki wa TanPower. Mkataba wa kampuni hiyo na TANESCO, unaeleza kampuni kulipwa kiasi cha dola 271 milioni (karibu Sh. 371 bilioni) katika kipindi chote cha uhai wa mkataba.

Si hivyo tu. Zitto hataki tujadili kutoonekana kwa mchango wa anayejiita mwekezaji mwenye asilimia 85 na badala yake serikali yenye hisa ndogo tu (asilimia 15).

Kifungu cha 13 cha kanuni kinataja kazi za kamati ya POAC kuwa ni kushughulikia taarifa za kila mwaka za hesabu zilizokaguliwa za mashirika hayo; na kushughulikia matatizo sugu yaliyoanishwa na mkaguzi wa serikali katika hesabu zake za kila mwaka.

Kazi nyingine, ni kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yaliyokwishatolewa na kamati, kutathimini ufanisi wa mashirika ya umma na kufuatilia utekelezaji wa sera ya ubinafsishaji wa mashirika hayo.

Kwa kuwa kazi ya Kamati ya Zitto ni kushughulikia taarifa za kila mwaka za hesabu zilizokaguliwa; ilitarajiwa kujadili kwanza jinsi fedha zilizotolewa zilivyotumika. Nani aliyeagiza kutolewa? Nani alizipokea? Kwa makubaliano yapi? Yupi aliyeelekeza matumizi yake?

Haya hataki tujadili. Badala yake, anasisitiza kuwa “kamati yangu” – ambayo haifanyi kazi za kamati za kisekta – inashauri na hata kuagiza serikali kukabidhi mgodi wa Kiwira kwa NSSF. 

Kwanza, kabla Zitto kupigia chapuo NSSF kukabidhiwa mradi wa Kiwira, angetaka kampuni ya TanPower kurejesha serikalini mabilioni ya shilingi waliyopewa na NSSF.

Zitto na wenzake wangetafuta na kujua, kama ilivyowekwa wazi sasa, kwamba fedha zilizotolewa hazikutumika kwa kazi iliyotarajiwa, kwa kuwa mitambo iliyotajwa kukarabatiwa haikufanyiwa ukarabati wowote.

Pili, Zitto angemtaka Mkapa aeleze kwa nini serikali yenye hisa ndogo ilitenga Sh. 17 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa mitambo, huku mwekezaji mwenye hisa nyingi akiwa hakutoa chochote.

Tatu, kabla Zitto kufanya kazi aliyotumwa angeeleza kwanza kwa nini kamati yake haielezi kilichosababisha serikali kumuacha mwekezaji anayedaiwa kung’oa baadhi ya mitambo na kuiuza kama chuma chakavu, lakini inaelezwa kuwa huko ilikouzwa inaendelea kuzalisha.

Aidha, Zitto ni miongoni mwa wapangaji wa NSSF katika nyumba zake zilizopo Tabata, wilayani Ilala, Dar es Salaam. Pamoja na chapuo anayofanya, hajatamka maslahi yake katika mradi huu. Bado tunafuatilia.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: