Zitto anataka kusaliti CHADEMA


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 24 November 2010

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi
Zitto Zuberi Kabwe

MKUTANO wa kwanza wa Bunge la kumi uliomalizika Alhamisi iliyopita, mjini Dodoma, umeandika historia.

Ni kwa wabunge wa chama kikuu cha upinzani nchini – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kususia hotuba ya rais Jakaya Kikwete na kutoka nje ya ukumbi wa bunge.

Hilo ni tukio la kwanza kumkuta rais wa Jamhuri tangu taifa hili lipate uhuru, miaka 50 iliyopita.

Wengi wamezungumzia tukio hilo, lakini wengi wao, wamejikita katika kulaumu CHADEMA.

Bali, tukio lile lina sura nyingi za kujadiliwa. Kwa mfano, kuna rais anayesusiwa; aliyejibu ususaji kwa njia ya vijembe na kejeli; na kuna wabunge waliozomea badala ya kusikitika.

Kuna waziri mkuu anayelaumu na kulaani badala ya kuchukua hatua kabla ya tukio lenyewe kutokea; kuna serikali iliyoshindwa kuongea na viongozi wa CHADEMA ili kumuepusha mkuu wa nchi na aibu iliyompata.

Yupo spika “mwanafunzi” ambaye ameshindwa kufanya jitihada zozote za wazi kuepusha aibu iliyotokea na ambayo imemfunika yeye na historia yake aliyoiweka siku chache zilizopita.

Kuna CHADEMA na uamuzi wa kutumia njia ya kususia badala ya kutumia nyingine kama kweli zilikuwepo. Vipo vyama vingine vya upinzani ambavyo badala ya kusikitika, viliinuka kuchukua viti vilivyoachwa wazi na CHADEMA.

Kwa ujumla, tukio lile lilikuwa na sura nyingi, lakini ushabiki wa baadhi ya waliojitosa kujadili, umewanyima wananchi wengi fursa ya kuchambua na kujadili sura hizo kwa faida ya vizazi vijavyo.

Makala hii, nayo haitajadili hayo. Badala yake, itajikita katika mjadala ulioibuliwa na mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), naibu katibu mkuu wa chama hicho na naibu kiongozi wa upinzani bungeni, Zitto Kabwe.

Yeye na baadhi ya wabunge wenzake wachache waliamua kutoingia bungeni kinyume na maelekezo ya chama chao.

Katika utetezi na ufafanuzi alioutoa kupitia televisheni ya taifa (TBC1), Zitto anadai pamoja na mengi, kuwa yeye na wenzake waliamua kutoingia ukumbini kuepuka kumwaibisha mkuu wa nchi ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu.

Kwamba, aliamua kufuata dhamiri na shinikizo la wapiga kura wake ili kuonyesha heshima kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye amefanya maendeleo makubwa mkoani Kigoma kuliko rais yeyote tangu uhuru.

Kwa Zitto, maendeleo mkoani Kigoma ni fadhila kutoka kwa rais na anajisikia deni mbele yake. Alihitimisha kwa kusema, “Rais ni alama ya umoja wa nchi na ni lazima aheshimiwe.”

Kabla ya utetezi wake, kulikuwa na taarifa kwamba Zitto alikuwa “anatumika” kushawishi wabunge wagawanyike katika suala la msimamo mmoja wa chama chao. Ilimlazimu kutumia hata udini ili kukamilisha adhima yake.

Kwa kuwa suala la udini alilizungumzia pia katika mahojiano yake na TBCI, nashawishika kuamini kuwa Zitto anayo ajenda ya udini katika kutimiza malengo yake ya kuigawa CHADEMA.

Iwe anayo yeye kama yeye, au anatumwa na wanaomtuma, kuna kila sababu ya kuamini kuwa Zitto ametekwa na fikra hizi mbaya za udini anaodai anaupinga.

Fikra hizi ni matusi kwa wananchi waliomchagua kutokana na kuamini kuwa ana uwezo wa kuongoza. Kumbe moyoni mwake anaamini kuwa alichaguliwa kwa misingi ya udini!

Kwa mwanasiasa kijana, msomi na aliyewahi kujijengea heshima siku za nyuma, hatua hii inawasaliti maelfu ya vijana waliokuwa na matumaini makubwa kwake, kwani wanaona kauli na vitendo vyake vinachonga jeneza lake na fikra zake.

Naendelea kumwamini hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyesema kuwa wanasiasa waliofilisika au wanaoelekea kufilisika, hujificha ndani ya kwapa la udini na ukabila.

Kwa hili, Zitto amefilisika mapema wakati biashara ya siasa ndiyo inaanza.
Siku mbili kabla ya tukio la bungeni, Zitto alikuwa na mazungumzo ya muda mrefu na alikuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na baadaye akafanya mazungumzo na Rais Kikwete kwa njia ya simu.

Habari hizi alizisema Zitto mwenyewe ili kuwashawishi wabunge wakubaliane naye katika “mpango” wake wa kukigawa chama chake.

Baadaye alikutana na “maofisa maalum” wa serikali aliodai kuwa walikuwa wanampa habari maalum za kusaidia kumaliza aibu ambayo ingetokea kwa kususia hotuba ya rais. Wanafahamika hata kwa majina.

Kwa ujumla, Zitto alionekana kumhurumia Kikwete kuliko hata Chama Cha Mapinduzi (CCM) chenyewe kinavyomhurumia mwenyekiti wake.

Kwa mtu yeyote anayejali na kupenda kuimarisha siasa mbadala katika nchi, atasikitika kusikia na kuona haya yakifanywa na Zitto.

Hata kama upinzani si uadui, lakini upinzani unaojipendekeza kwa CCM kuliko hata wana-CCM wenyewe ni wa hatari; na wanachama wenyewe wa CCM hawautaki.

Wana-CCM makini hawapendi tabia ya Zitto kujipendekeza kwa viongozi wa juu na wakati mwingine kuwachonganisha kwa kuvujisha habari azipatazo kutoka kwa mmoja kwenda kwa mwingine.

Tayari hatua ya Zitto ya kuchukua maneno ya huyu na kumpa yule, imechochea mgogoro wa chinichini ndani ya chama cha Kikwete.

Mgogoro huu unapata nguvu kutokana na utamaduni mpya wa mtendaji mkuu wa CCM, Yusuph Makamba kuthamini wapinzani mamluki wanaorejea CCM baada ya kuwa wameshakibomoa chama hicho kwa kukishushia lundo la shutuma.

Orodha ya wanaopewa kipaumbele na Makamba kuliko wanachama wengi wanaojitolea kujenga chama chao, inahusisha Steven Wasira, Tambwe Hizza, Mbarouk Msabaha, Dk. Amani Kaborou, Sahibu Akwilombe, Daniel Nsanzugwanko, Justine Sarakana na Thomas Ngawaiya.

Ndani ya chama cha Makamba na Kikwete, hawa ni wanachama wanaotoka daraja tofauti.

Naye Zitto anaelekea kupenda kujiunga na orodha hiyo kwa gharama mbili kubwa. Kwanza, kwa kuigawa CHADEMA (yenyewe kwa yenyewe) na pia CHADEMA na wapinzani wengine.

Pili, anaelekea kuanzisha migogoro ya ndani ya CCM kwa sababu anadai anayoyafanya ndani ya CCM anakuwa na ridhaa ya kiongozi mkuu wa chama – Makamba.

Wenye akili wanajua kuwa baadhi ya madai yake si ya kweli. Lakini hata yale machache yaliyo ya kweli, hayana dhamana ya chama hicho, bali utashi binafsi wa mmoja wa viongozi ndani ya chama hicho.

Katika suala la uadilifu kwa chama, CCM ikiwa taasisi, haina mwanachama aliye juu ya sheria hata kama wapo watu wengi nje ya chama hiki ambao wanaweza kupinga dai hili.

Kwa mfano, sidhani kama Zitto ana thamani kubwa ndani ya CCM kuliko Lowassa ambaye pamoja na mengi makubwa aliyokifanyia chama chake, bado wamegoma kumsafisha kutoka katika tuhuma zilizosababisha ateme kiti chake cha uwaziri mkuu.

Wala sidhani kama Zitto ni bora kuliko Samweli Sitta ambaye licha ya kuweka rekodi nzuri ya kusimamia bunge, ni CCM iliyosema Sitta hafai tena kuwa spika.

Ni Sitta na Lowassa waliofanikisha “kampeni za kisayansi” zilizomwingiza Kikwete madarakani mwaka 2005, lakini ni Kikwete huyohuyo aliyesema Sitta hafai na anaelezwa kila siku hadi asadiki kuwa Lowassa hasafishiki.

Mifano hii inatosha kumfundisha Zitto kuwa yuko hatarini pale anapojifanya na kudai kumheshimu mwenyekiti wa CCM kuliko anavyomheshimu mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Usaliti ambao Zitto anaufanyia CHADEMA ni huohuo atakaoifanyia CCM endapo atajiunga na chama hicho.

Inavyoelekea si siku nyingi kutoka sasa Zitto atajisajili katika CCM ambayo anaitumikia sasa kwa mlango wa nyuma.

Nitakuwa wa mwisho kumkaribisha Zitto ndani ya CCM. Chama cha CCM kiko tayari kumtosa yeyote hata kama kwa kufanya hivyo kinapata hasara.

Zitto hajachelewa kuachana na utoto huu kwa kuheshimu chama chake ambacho, siyo tu kinaheshimiwa bali hata kuogopwa na wengi wakiwamo baadhi ya viongizi wakuu wa CCM.

Vinginevyo, Zitto awe tayari kuangamia.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: