Zitto ayumbisha CHADEMA


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 01 December 2010

Printer-friendly version
ZITTO Kabwe

ZITTO Kabwe, sasa anatuhumiwa kuyumbisha chama chake kwa kukiingiza katika mahusiano ya mashaka.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto anafanya mawasiliano nje ya chama ambayo wachunguzi wameeleza yanaweza kukigawa na kukiangamiza.

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam zinasema licha ya kuwa na uhusiano wa karibu na baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi, Zitto “anajipendekeza kwa Rais Jakaya Kikwete.”

Ndani ya mwaka mmoja sasa, Zitto amekuwa na mahusiano ya karibu na baadhi ya watuhumiwa wa ufisani pamoja na kujipendekeza kwa rais Kikwete, jambo ambalo limeibua maswali mengi.

Waziri mmoja mwandamizi katika serikali ya Rais Kikwete ameliambia gazeti hili kuwa “kujikomba kwa Zitto kwa rais” kumelenga kugombanisha baadhi ya mawaziri na rais na mawaziri kwa mawaziri.

“Huyu bwana mdogo, anachukua maneno huku anapeleka kule. Mara ameomba uwaziri. Mara hivi…Mara vile, ili mradi ni shida. Kuna siku rais alisikika akisema, “Kwa nini huyu bwana mdogo asiimarishe chama chake, kuliko haya anayoyafanya,” ameeleza waziri huyo kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Katika mawasiliano yake, Zitto amejipa kazi ya kushauri Rais Kikwete katika masuala yanayohusu kampuni ya upakuaji makontena bandarini (TICTS).

Tarehe 25 Aprili mwaka jana, Zitto alimpelekea Rais Kikwete barua ikisema, pamoja na mambo mengine, “…ninaleta kwako ushauri ufuatao ili kumaliza suala hili kabisa bila ya kuathiri sura (image) ya nchi katika uwekezaji duniani na pia kuongeza ufanisi wa bandari.”

Kwanza, Zitto anasema, “Serikali ikubaliane na TICTS kuondoa kipengele cha exclusivity (hodhi ya biashara) katika mkataba wake ili kuruhusu ushindani na hivyo kuongeza ufanisi; na zabuni ya kuendesha kitengo kingine cha makontena katika Berths 13 & 14 itangazwe kwa kufuata sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2004.”

Pili, “Serikali itangaze rasmi kuwa nyongeza ya mkataba na TICTS itaendelea kwa sababu uwekezaji katika miundombinu ya bandari ni ya muda mrefu na hivyo mkataba wa mwanzo wa miaka 10 haukuwa na mantiki kiuwekezaji.”

Mapendekezo ya Zitto ya kutaka serikali isivunje mkataba, yanafanana na yale ambayo serikali ilitekeleza, pamoja na zogo kubwa kuibuka ndani na nje ya Bunge.

Katika mawasiliano hayo, Zitto anaeleza kuwa kilichoandikwa ni siri kati yake na serikali na rais.

Hata hivyo, siku tatu baadaye, Zitto alipeleka nakala ya barua aliyompelekea rais, kwa mtendaji mkuu wa kampuni ya Vertex International Securities, Peter Machunde.

Nakala hiyo ya barua kwa rais aliituma kwa Machunde, Jumanne 28 Aprili 2009, saa 3:45 asubuhi ikiwa na maneno, “This is for me and you only (Hii ni kwa ajili yako na mimi tu) ambayo nimepeleka kwa mkuu wa nchi.”

Machunde ni swahiba mkuu wa kibiashara wa mmoja wa watuhumiwa wa ufisadi nchini, Nazir Karamagi ambaye ni mmoja wa wamiliki wa TICTS.

Mara kadhaa CHADEMA imemtuhumu Karamagi kuingiza nchi katika mikataba ya kinyonyaji ya madini hasa mkataba wa Buzwagi.

Mkataba huo uliosainiwa nje ya nchi na Karamagi, ulizua zogo kubwa bungeni hadi kusababisha Zitto kusimamishwa ubunge kwa muda.

MwanaHALISI limeshindwa kuthibitisha dhamira ya Zitto katika kutuma barua moja kwa rais na kwa watu wa TICTS, na alipoulizwa kwanini aliamua kufanya hivyo, Zitto alijibu:

“Kama mmeamua kuichapa hiyo habari, go ahead. I have no comment” – (endeleeni tu, sina cha kusema).

Mbali na mawasiliano na baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi, Zitto amedaiwa kuwa na tabia ya kuwasiliana na baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari na kujiandikia habari huku wao wakitakiwa “kuzichapa kama zilivyo.”

Kwa mfano, katika mawasiliano yake na mmoja wa wahariri wa gazeti moja linalotolewa kila siku nchini (jina tunalo), Zitto anaeleza:

“…hii ripoti inapaswa kusomwa siku ya Jumatano. Nimekutumia wewe pekee. So I expect a build up siku ya Jumatano bila kutoa details na stori ya Alhamisi iandaliwe vizuri na kwa muda mrefu labda ikiwemo na Q and A (maswali na majibu) na mimi katikakati katika kutoa elaboration (ufafanuzi). Yaani tufanyie splash (tutandaze) mbele with issues and graphs (kwa hoja na grafu).”

Akiandika na kuagiza kama mhariri wa gazeti, Zitto anasema, “Jumatano yaweza kuwa na stori,” huku akipendekeza kichwa cha habari kuwa ‘Zitto ana siri nzito…’

Anasema, “Nadhani ukishanifanyia editing (uhariri) nimpe na …kwa story building (mkuzo/uimarishaji wa stori) maana yeye ataikosa …Pia tumpe na …. Hao tu.” (Majina ya anaotaka kuwapa habari tunayo).

Zitto anaeleza kwa njia ya baruapepe, “Nataka pia IPP media wakose kabisa na wasikie ukumbini tu ili wasikie uchungu na waendelee na maspin yao ya kina Kilango (Anne Kilango Malecela, mbunge wa Same Mashariki).”

Mawasiliano kama hayo aliwahi kuyafanya na mhariri mwingine wa gazeti la kila siku (jina tunalo), siku mbili kabla ya rais Kikwete kuhutubia Bunge.

Katika mawasiliano yake kwa mhariri huyo Zitto anasema, “…Nimekutumia hii nyaraka, naomba uifanyie kazi. Lakini kesho unaweza kuwa na stori: Muundo wa Baraza la mawaziri. Kikwete kushirikisha wapinzani. Tamko la CHADEMA latibua.”

Katika hatua nyingine, Zitto anatuhumiwa kuwa na mawasiliano ya karibu ya kikazi na binafsi, na Maria Kejo, mtumishi wa serikali katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), anayetuhumiwa na CHADEMA katika kashfa kadhaa nchini.

Uongozi wa CHADEMA unamtuhumu Kejo kutoa ushauri uliowezesha kufikiwa kwa makubaliano yaliyozaa mkataba wa kufua umeme wa Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ambao ni katili na matokeo yake ni mzigo usiobebeka wa gharama ya umeme.

Msingi wa ushauri huo ni kwamba mkataba ulifungwa kutokana na shinikizo la rushwa zilizotolewa kwa baadhi ya watendaji serikalini.

Hati ya kiapo ya Patrick Rutabanzibwa, ambaye alikuwa Kamishina wa Nishati na Madini, inathibitisha alikataa kuhongwa dola za Marekani 200,000.

Katika mawasiliano yake ya imeili na Kejo ya 23 Aprili 2009, Zitto anaonekana kumtumia Kejo mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) kuhusu mkataba kati ya serikali na IPTL.

Kwa mujibu wa mawasiliano hayo, Zitto anamueleza Kejo, “…Pitia kisha ushauri katika mambo ya IPTL na Benki Kuu. Pia pengine popote utakapoona inafaa kushauri.

“Tunaisoma Jumatano na ni draft (rasimu) bado, but strictly confidential. Can come to your office (lakini hii ni siri kubwa, naweza kuja ofisini kwako kuzungumza,” ananukuliwa Zitto akiandika katika imeili.

Akiandika kwa kujiamini, Zitto anasema, “Halafu sina hela mpenzi…” Mawasiliano hayo yalifanyika saa 10:59 alfajiri na Zitto alipendekeza wakutane na “swahiba” wake huyo jioni ya siku hiyo.

Imeili hiyo inaonyesha kwamba Zitto alikuwa amempa mama huyo rasimu ya hotuba ambayo alitakiwa kuiwasilisha bungeni wiki iliyofuata.

Jingine ambalo Zitto alitaka kutoka kwa Kejo, ni juu ya kushughulikia wizi wa mabilioni ya shilingi ndani ya Benki Kuu ya taifa (BoT). Mbali na IPTL, Kejo anatuhumiwa kunyamazia wizi ndani ya BoT.

Alipoulizwa na MwanaHALISI kwa njia ya simu kuhusu mawasiliano yake na Kejo na uhusiano wao umelenga nini, Zitto alijibu haraka, “Mama Maria Kejo alikuwa mjumbe wa kamati ya rais ya madini ambayo mimi pia nilikuwa mjumbe. Kwamba kuna mawasiliano kuhusu IPTL na BoT kati yangu na yeye sijui na sina la kujibu.”

Wiki iliyopita, Zitto alikiambia kituo cha televisheni cha TBC1 kuwa hakubaliani na uamuzi wa chama chake kususia hotuba ya Rais Kikwete wakati wa kufungua Bunge la 10.

Kauli ya Zitto inadaiwa na wanachama wa CHADEMA kuwa tofauti na ile aliyotoa katika vikao vya sektarieti na kwamba “inalenga kuleta mtafaruku” ndani ya chama chao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: