Zitto na kauli tata


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 13 January 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala
Zitto Kabwe

MBUNGE wa Chadema katika jimbo la Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ameibua mjadala mwingine. Anasema siasa halikuwa "chaguo la kwanza" katika maisha yake.

Bali Zitto anasema, “nimeingia katika siasa kwa bahati mbaya,” na kwamba kazi anayoipenda zaidi ni ualimu. Anajiandaa kwa kazi hiyo.

Alitoa kauli hiyo katika mahojiano aliyofanya na kituo cha televisheni cha TBC1 na kunukuliwa na vyombo vingine vya habari tarehe 4 Januari 2010.

Kauli ya Zitto, imekuja takribani miezi mitano tangu kumalizika kwa kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu ndani ya chama chake. Yeye aligombea nafasi ya uenyekiti.

Hii si mara ya kwanza kwa Zitto kutoa kauli zenye utata. Wakati mwingine kauli zake zinatofautiana hata na msimamo wa chama chake.

Ni kweli kuwa Zitto ni mtu huru. Aweza kuamua na kutenda atakacho. Lakini huyu ni kiongozi. Ni kioo ndani ya chama na jamii. Kauli yake yoyote inachukuliwa kwa uzito unaostahili ndani na nje ya chama chake.

Wiki iliyopita, mshiriki wa kongamano la wanachuo wa Chadema, Owawa Steven alisema wengi wa vijana waliohudhuria kongamano walivutika na mwelekeo wa Zitto.

Sasa swali muhimu la kujiuliza ni hili: Kwa nini Zitto anapenda kuzungumza vitu ambavyo vinazua mjadala unaoweza kuangamiza kisiasa hata yeye mwenyewe?

Kwa mfano, kama Zitto anasema “siasa halikuwa chaguo lake la kwanza,” kwa nini aligombea uenyekiti wa Chadema kumpinga Freeman Mbowe?

Alitaka kugombea ili iweje? Kwa faida ya nani? Nani alishinikiza Zitto kugombea nafasi hiyo?

Je, alitaka akishinda afanye nini? Angelipa nini wale waliomsukuma kugombea – kama hakuwa amegombea kwa utashi wake?

Maswali yaweza kuwa mengi. Kwa mfano, wengine wangeuliza: Aligombea kwa lengo lipi? Kuvuruga Chadema au kuimarisha?

Mapema mwaka jana Zitto alishinikiza serikali kununua mitambo ya kampuni ya kitapeli ya Richmond/Dowans hadi kuibua mjadala mpana ndani na nje ya Bunge.

Alitenda hivyo huku akijua kuwa msimamo wa chama chake, ni kutaifishwa kwa mitambo hiyo.

Hata pale Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dk. Idris Rashid walipotangazia ulimwengu kuwa wamesitisha mpango wa kununua mitambo hiyo, bado Zitto aliendelea kung’ang’ania mitambo inunuliwe, kana kwamba taifa zima linamulikwa na Dowans.

Zitto alitenda yote hayo huku akijua kwamba Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA) ya mwaka 2004 katika kifungu cha 58 (3) inakataza kabisa ununuzi wa mitambo chakavu.

Majuzi, Zitto amenukuliwa akimtetea David Kafulila, aliyekuwa “karani” katika kurugenzi ya habari ya Chadema.

Kafulila alienguliwa katika nafasi yake kutokana na kile Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa alichoita, “utovu wa nidhamu.”

Tayari Kafulila ametimkia chama cha NCCR- Mageuzi. Lakini Zitto anasema atakufa na Kafulila na atatumia kila uwezo wake kuhakikisha anatingia bungeni kabla ya John Mnyika, mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chadema.

Hii ina maana kwamba Zitto yuko tayari kusaliti hata chama chake, iwapo kitaamua kusimamisha mgombea katika jimbo la Kigoma Kusini ambako Kafulila anatajwa kugombea.

Kama hivi ndivyo Zitto anavyotenda na kuamini, inawezekana kuwa hakustahili kuwa mwanasiasa, na kwamba aliingia katika kapu hilo kwa bahati mbaya. Tusubiri mwisho wake tuone!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: