Zuma kama Kikwete, Mkapa kama Mbeki


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 21 April 2010

Printer-friendly version
VITENDO, si maneno, ndivyo huwafanya wananchi wamwamini kiongozi wao - Mac Maharaj

AKIANDIKA katika gazeti la Mail&Guardian la Afrika Kusini Mei mwaka jana, mwanahistoria na mchambuzi wa masuala ya siasa wa nchi hiyo, William Gumede, alisema ifuavyo kumhusu Rais Jacob Zuma:

“Msholozi (jina la kikabila la Zuma kama ilivyo Madiba kwa Nelson Mandela) amepata ushindi mkubwa si kwa sababu ya sera au utendaji kazi wake. Ameshinda kwa sababu wananchi wamejenga imani juu yake kuwa anajua matatizo yao.

Bahati yake mbaya ni kwamba wananchi haohao waliompa kura jana, watamnyima kura kesho iwapo hawatapata wanachokitarajia kwake.”

Nyumbani Tanzania, Rais Jakaya Kikwete aliingia madarakani bila ya kuwa na jambo lolote la kuonyesha kuwa alikuwa anawazidi washindani wake katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi hiyo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kama kigezo ilikuwa ni utumishi wake wa miaka 10 kama mwanadiplomasia wakati wa uongozi wa rais Benjamin Mkapa, basi hakikutosha kwani wengi tunajua Dk. Salim Ahmed Salim amebobea katika anga hiyo mara nyingi zaidi yake.

Kama kigezo ilikuwa ni utumishi wake ndani ya serikali na chama, inajulikana wapo watumishi wengi waliotumika muda mrefu zaidi ndani ya chama na serikali kuliko yeye.

Kikwete alikuwa na bahati ya kupendwa tu na wananchi baada ya kubebwa na baadhi ya vyombo vya habari na waandishi wa habari mmojammoja. Walimuona kama mtu anayefahamu shida na matatizo yao.

Na kama ilivyokuwa kwa Zuma, Kikwete pia alipata bahati (mbaya na nzuri) ya kuwa na timu ya kampeni iliyokuwa tayari kufanya lolote ili kuhakikisha anaingia madarakani.

Ninaamini timu hii (kundi hili), haikuwa na dira wala mwelekeo wa nini kitafanyika baada ya mgombea wao kupata urais. Kwao, lililokuwa muhimu ni kumwingiza tu madarakani.

Kwa wasomaji wanaofuatilia taarifa za kihabari za nchini Afrika Kusini, bila ya shaka itakuwa wamesikia habari za mwanasiasa kijana wa nchi hiyo, Julius Malema. Huyu ni Rais wa Umoja wa Vijana wa chama cha African National Congress (ANC) anachotoka rais Zuma.

Malema ambaye kwa baadhi ya magazeti yanamuita kwa ufupi Juju, alitangaza kumuunga mkono Zuma wakati wa mchakato wa kupatikana kwa rais mpya.

Ukinara aliochukua wakati wa harakati za ANC kutafuta kiongozi wa kumrithi rais Thabo Mbeki, unafanana na ule aliouchukua Emmanuel Nchimbi wakati wa harakati za CCM kutafuta mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Nchimbi alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UV-CCM) na alimuunga mkono Kikwete kwa nguvu kubwa.

Tofauti kati yao wakati wa harakati za vyama vyao kutafuta mgombea urais, ni moja: Malema alithubutu kusema wazi kwamba yuko tayari kuua au kuuawa kwa ajili ya Zuma. Alirudia matamshi hayo mara kadhaa.

Kama ilivyokuwa kwa Kikwete na wafadhili wake wa kampeni, Zuma pia alikuwa na watu wake: wafanyabiashara wenye utata.

Juu ya wachangiaji wake wote wakubwa, walikuwapo watu kama Shabir Schaik na Tokyo Sexwale, ambao wanakabiliwa na tuhuma mbalimbali za kifisadi kabla ya Zuma kupata urais. Tuhuma hizo zinaendelea.

Watu kama Malema na Shabir wanamletea Zuma matatizo makubwa hivi sasa. Suala hili nitalijadili vizuri huko mbele twendako katika mfululizo wa mjadala huu. Kwa sasa, nataka kujiweka zaidi katika suala la watangulizi wa Kikwete na Zuma.

Ni jambo la wazi kwamba Thabo Mvyelwa Mbeki hakupenda arithiwe kiuongozi na Zuma. Alitaka aendelee na urais kwa kipindi cha tatu au achague mtu anayemtaka ndiyo awe rais wa Afrika Kusini, taifa lenye uchumi mzuri, lakini nguzo zake kuu zikiwa bado mikononi mwa wafanyabiashara wa Kizungu.

Ndiyo maana kuna madai kwamba hata tuhuma mbalimbali zilizokuwa zikitajwa juu ya Zuma - hasahasa za kuwa mpenda wanawake sana (mwasherati) na ufisadi zilitengenezwa na serikali ya Mbeki ili kumharibia.

Zuma alifanikiwa kuvuka vikwazo vyote vilivyolenga kumkwamisha. Jitihada na mikakati ya watu kama Malema na Tokyo zilichangia sana.

Walimpigania hadi dakika ya mwisho afuzu kuwa rais. Walijenga taswira na kuikomaza kwa umma wa wana wa ANC na wananchi wengineo ya kuonyesha kuwa Msholozi anaonewa.

Hata hivyo, mara baada ya kuingia madarakani, Zuma ameongeza mke mwingine Thobeka Madiba na hivi sasa anatuhumiwa kutembea na mtoto wa rafiki yake Irvin Khoza aitwaye Sonono na wamezaa mtoto mmoja nje ya ndoa. Tayari Zuma amewasilisha mahari kwa ajili ya kumoa Sonono.

Kuna habari kwamba Mkapa hakutaka Kikwete awe mrithi wake. Upo mtizamo ulioonyesha kwamba chaguo lake halisi lilikuwa ni Dk. Abdallah Kigoda, mbunge wa Handeni mkoani Tanga ambaye alikuwa mfuasi wake mkubwa katika sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma na uchumi wa soko huria.

Hata hivyo, Mkapa alikuwa na busara ya kusoma alama za nyakati. Baada ya kutazama wimbi linavyokwenda, aliamua dakika za mwisho, kumuunga mkono Kikwete kama ilivyoonekana wakati wa maelezo yake kabla ya wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM kupiga kura ya mwisho kuchagua mgombea.

Vinginevyo, kwa maana zaidi ya moja, utendaji kazi na tabia za Mkapa na Mbeki unafanana sana.

Kwa watu weusi wengi nchini Afrika Kusini, Mbeki alikuwa mtu anayejiona bora kuliko wenzake, mshaufu na anayeeleweka zaidi na wasomi na wazungu kuliko na weusi wenzake.

Kama ambavyo mara nyingi Mkapa alikuwa na migogoro na vyombo vya habari na waandishi wa Tanzania, hali ilikuwa hivyohivyo kwa Mbeki nchini kwake.

Mbeki alitumia muda mwingi kusuluhisha migogoro ya DRC, Burundi na Ivory Coast. Alitumia muda mwingi kutengeneza mpango wa NEPAD na kuitengeneza Afrika Kusini kama mdau mkubwa katika anga za kimataifa.

Tatizo ni kwamba wengi wa wananchi wa Afrika Kusini wana uelewa mdogo sana wa masuala yaliyo nje ya nchi yao. Wao walitaka ajira na makazi bora. Hivyo ndio vipaumbele vyao na siyo migogoro ya Afrika na NEPAD.

Ni sawa na namna ambavyo Mkapa alikuwa akijishughulisha na mambo ya utandawazi na Tume ya (Tony, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza) Blair kuhusu Afrika ambavyo Watanzania hawakuona umuhimu wake.

Lakini, tofauti na Mandela ambaye alipendwa kwa sababu tu ya historia yake ya mapambano dhidi ya ubaguzi na namna alivyounganisha nchi, Mbeki alifanya mambo makubwa kwa nchi.

Ni wakati wa Mbeki serikali ilianzisha mkakati maalum wa kuwawezesha watu weusi (BEE). Watu kama Patrice Motsepe, Irvin Khoza na Sexwale mwenyewe ni wafaidikaji wa mpango huo.

Pamoja na wananchi kutompenda, Mbeki aliinua uchumi kwa ushirikiano mkubwa na Waziri wa Fedha, Trevor Manuel na Gavana wa Benki Kuu ya Afrika Kusini, Tito Mboweni.

Sawa tu na Mkapa kwa namna fulani. Pamoja na lawama zote anazotupiwa, alifanikiwa kujenga uchumi. Alijenga miundombinu, alidhibiti mfumuko wa bei na aliishibisha akiba ya taifa ya fedha za kigeni.

Wiki ijayo nitaeleza namna kile kinachoendelea Afrika Kusini sasa kilivyo na uhusiano mkubwa na tunayoyashuhudia nchini.
0
No votes yet